Dunia TV ni jukwaa la kidigitali linalobeba taswira ya ubunifu wa Kitanzania kwa njia ya kipekee. Ni programu ya simu iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya watanzania na wapenzi wa tamaduni za Kiafrika wanaotaka kupata filamu, vipindi na maudhui mengine ya ndani kwa urahisi na ubora wa hali ya juu. Tofauti na majukwaa ya kimataifa, Dunia TV imejikita katika kukuza na kuendeleza kazi za wasanii wa Tanzania kwa kutoa nafasi ya kusikilizwa na kutazamwa na hadhira kubwa, huku ikihifadhi mila, simulizi na mitindo ya maisha inayotambulisha utambulisho wetu wa taifa.
Kwa mtindo wake wa kipekee, Dunia TV inafanya kazi kwa mfumo wa uanachama ambapo mtumiaji hulipia kwa gharama nafuu ili kupata ufikiaji wa maudhui yote bila vikwazo. Tofauti na baadhi ya majukwaa makubwa, Dunia TV haina kipengele cha kudownload video, jambo linalolenga kulinda kazi za wasanii dhidi ya usambazaji holela na kuhakikisha ubunifu unathaminiwa ipasavyo. Watumiaji hupata burudani moja kwa moja kupitia mtandao, wakifurahia ubora wa picha na sauti kulingana na kasi ya intaneti waliyonayo.
Maudhui yaliyopo ndani ya Dunia TV yanajumuisha filamu ndefu, tamthilia fupi, vipindi vya familia, makala za kijamii na tamaduni, pamoja na michezo ya kuigiza inayohusiana na maisha ya kila siku ya Mtanzania. Lengo kuu ni kutoa burudani halisi inayogusa hisia na maisha ya watu, huku ikiwapa nafasi wasanii chipukizi na wabunifu wa ndani kupata jukwaa la kitaifa na kimataifa. Kwa njia hii, Dunia TV sio tu huduma ya kutazama filamu, bali pia ni injini ya maendeleo ya sekta ya sanaa na utamaduni.